Posts

Showing posts from April, 2018
Image
Mamia ya wanawake waliotelekezwa baada ya kuzalishwa na waume zao wamejazana katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyetangaza kuanza kuwasikiliza. Kumekuwa na mafuriko ya wanawake wanaoingia kwa kusukumana kwenye ofisi hizo hali iliyowalazimu walinzi kufunga geti ili walio ndani wahudumiwe. Wanasheria na wafanyakazi wengine wa ofisi hiyo wanaendelea kuwasikiliza wanawake hao wengi wao wakiwa wamebeba watoto wao. Wakizungumza na MCL Digital leo, Aprili 9 wanawake hao wamesema wingi wao unaweza kusababisha baadhi yao kushindwa kusikilizwa. "Nilitelekezwa na watoto wanne kwenye nyumba ya kupanga, nimekuwa kama ombaomba nashukuru Makonda ameona kilio chetu lakini kwa umati huu naogopa sana,"amesema mwanamke mmoja. Wapo waliolala kwenye ofisi hizo huku wengine wakianza kuwasili tangu saa tisa za usiku.  Vimetengwa vyumba maalum zikiwamo kumbi zilizo katika ofisi hizo kwa ajili ya kusikiliza kilichowasibu wanawake hao.

Idadi ya wafungwa Tanzania kuzidi uwezo wa magereza

Image
Tanzania inakadiriwa kuwa na wafungwa 40,000 wakati uwezo wa magereza yake ni 30,000 hivyo kuna ongezeko la zaidi ya wafungwa 10,000 katika msongamano huo. Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Hamad Yusufu Masauni wakati akijibu swali la nyongeza la Ruth Mollel ambaye ametaka kujua Serikali inafanya nini kumaliza msongamano wa wafungwa. Masauni amesema kuna ongezeko la zaidi ya wafungwa 10,000 ambapo kwa sasa Serikali inafanya kila namna kumaliza msongamano huo. Katika swali la msingi Mwantakaje  Haji Juma  (BUBUBU-CCM) amehoji ni lini kituo cha polisi katika jimbo lake kitafanyiwa ukarabati. Naibu Waziri amesema kituo hicho kitafanyiwa kazi wakati wowote fedha ikipatikana ili kiwawezeshe askari kutoa huduma bora.